Tuesday, September 07, 2010
   
Text Size

Site Search

Blatter amuonya rais Sarkozy

*Aziomba radhi FA za England, Mexico kutokana na makosa ya waamuzi
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
RAIS wa FIFA, Sepp Blatter ameonya kuwa Ufaransa inaweza kufungiwa kushiriki soka la kimataifa iwapo serikali itaingilia uendeshaji wa timu ya taifa.
Blatter alisema ametuma "ujumbe wa wazi” kwa Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, aliyeishutuma timu ya Ufaransa kwa kuonyesha kiwango cha chini kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Sarkozy aliahidi kuongoza uchunguzi wa kilichosababisha timu hiyo kuboronga.
Lakini Blatter alisisitiza mabosi wa soka duniani, Fifa, inapinga: "… uingiliaji wa kisiasa, hata kama ni katika ‘level’ ya urais."
Ufaransa ilimaliza ikiwa ya mwisho kwenye kundi lao huku ikiandamwa na matatizo ya ndani na nje ya uwanja.
Mshambuliaji Nicolas Anelka alitimuliwa kikosini baada ya kugoma kumwomba radhi kocha Raymond Domenech waliyebadilishana maneno makali.
Kikosi kilichosalia kiligomea mazoezi kupinga kutimuliwa kwa Anelka huku nahodha Patrice Evra akitukanana na kocha wa viungo, Robert Duverne.
Sarkozy aliamuru kufanyike marekebesho makubwa ndani ya FA ya nchi hiyo (FFF) na tangu timu irejee, amekwishafanya mazungumzo na nahodha wa zamani, Thierry Henry, huku Jean-Louis Valentin akiachia nafasi ya urais ya FFF.
FFF imekwisha omba radhi kwa mashabiki lakini Blatter alisema uingiliaji wa serikali katika masuala ya soka, hautavumiliwa.
"Ufaransa wanafanya mazungumzo na serikali lakini soka lazima libaki mikononi mwa shirikisho. Tutawasaidia kutatua hili na ikishindikana, tutaifungia nchi hiyo.
"Niseme wazi, kuingiliwa na siasa kwenye soka kutashughulikiwa na Fifa bila kujali serikali imeingilia namna gani au hata ukubwa wa nchi husika,” alisema Blatter. 
Wakati huo huo, Blatter ameiomba msamaha FA ya England kutokana na kukataliwa kwa bao la Frank Lampard.
Bao hilo la wazi lilikuwa la kusawazisha katika pambano la Kombe la Dunia hatua ya 16 bora dhidi ya Ujerumani wakati Ujerumani ikiongoza kwa mabao 2-1.
Shuti la mbali la Lampard liligonga mtambaa panya na kudunda ndani ya mstari wa goli lakini waamuzi wakalikataa na sekunde chache baadaye, marudio ya TV yalionyesha kuwa lilikuwa halali.
"Na sasa ni wazi kutokana na matatizo tuliyoyashuhudia kwenye Kombe la Dunia, itakuwa ni upuuzi kutoanzisha mjadala wa matumizi ya teknolojia wakati tutakapokutana Julai,” alisema Blatter.
Alikiri kuwa amekwisha zungumza na FA za England na Mexico kuhusu makosa ya waamuzi yaliyozigharimu timu zao na kuwaomba msamaha.

More Latest News

  • 1
  • 2
  • 3
  • 4

cartoons



Who's Online

We have 13 guests online

Login Form