Tuesday, September 07, 2010
   
Text Size

Site Search

Hispania yaweka historia


HISPANIA imekuwa taifa la nane kushinda Kombe la Dunia baada ya jana usiku kuifunga Uholanzi 1-0 katika mchezo mkali wa fainali uliochezwa Uwanja wa Soccer City jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Bao pekee la ushindi lilifungwa na kiungo mchezeshaji Andrea Iniesta dakika ya 116 muda wa ziada kwa kuachia shuti kali ndani ya bozi la penati baada ya kupokea pasi ya Cesc Fabregas. Kipigo hicho kilionekana kuwaumiza moyo zaidi wachezaji na mashabiki wa Uholanzi ambao walicheza pungufu baada ya beki wa kati John Heitinga kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Hii ni mara ya tatu kwa Uholanzi kupoteza mchezo wa fainali Kombe la Dunia baada ya mwaka wa 1974 kufungwa na iliyokuwa Ujerumani Magharibi na mwaka 1978 na Argentina. Hispania inaweka historia sawa na Ujerumani Magharibi mwaka wa 1974 pale walipochukuwa Kombe la Ulaya na Kombe la Dunia. Mchezo wa jana ulishuhudia mwamuzi wa kati kutoka England, Howard Webb, akionyesha kadi 13 za njano na moja nyekundu. Uholanzi walionyeshwa kadi nane za njano huku Hispania wakipata kadi nne. Tofauti na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya Ujerumani na Uruguay juzi ambao mabao tano yalifungwa, mechi ya jana usiku ilionekana wachezaji wa pande zote mbili wakicheza kujihami zaidi. Hata hivyo kadri muda ulivyokuwa unasonga mbele, Hispania walianza kuutawala mchezo huku Uholanzi wakionekana wanacheza rafu jambo ambalo lilisababisha Webb kuonyesha kadi nyingi za njano upande moja. Nusura Hispania wapate bao la kuongoza dakika tano tu ya mchezo lakini mpira wa kichwa uliopigwa na Sergio Ramos kutokana na krosi ya Xavi kudakwa na Maarten Stekelenburg. Kipindi cha pili, Uholanzi walipata nafasi ya wazi ya kufunga dakika ya 62 lakini shuti la Arjen Robben liliokolewa na kipa wa Hispania Iker Casillas. Dakika 10 za mwisho za mchezo zilishuhudia shuti la David Villa likizuiwa katika mstari, Ramos akipiga mpira wa kichwa nje na Carles Puyol kuwa na bahati ya kutoonyeshwa kadi baada ya kumzuia Robben akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga. Huku mashabiki wengi wakidhani finali hizo za kwanza Afrika zitaamuliwa kwa matuta, Iniesta alipokea mpira kutoka kwa Fabregas na mabeki wa Uholanzi wakidhani ameotea, aliachia shuti laki kwa guu lake la kulia lilomshinda Stekelenburg kudaka. Shamrashamra za sherehe za kufunga Kombe la Dunia ambao wasanii maarufu kama vile Shakira na Lady Blacksmith Mambazo walitumbuiza, zilihudhuriwa na Rais Mstaafu Nelson Mandela. Uholanzi: Stekelenburg, Van Der Wiel, Heitinga, Mathijsen, Van Bronckhorst, (Braafheid), Van Bommel, De Jong, (Van der Vaart), Sneijder, Kuyt (Elia), Van Persie, Robben. Hispania: Casillas, Pique, Puyol, Capdevila, Sergio Ramos, Iniesta, Xavi, Alonso (Fabregas), Busquets, Villa (Torres), Pedrito (Jesus Navas).

More Latest News

  • 1
  • 2
  • 3
  • 4

cartoons



Who's Online

We have 13 guests online

Login Form