Majigambo ya Karamagi yanatoka wapi?
Na Ibrahimu Rwamulaza
GAZETI la Rai toleo namba 871 la Juni 3-9, 2010, lilikuwa limepambwa na habari ya majigambo ya Mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi, iliyokuwa na kichwa cha habari cha ÒNitarudi Bungeni kwa kishindoÓ. Majigambo hayo yametokana na mahojiano aliyofanyiwa mbunge huyo na mwandishi Livingstone Ruhere na kupewa nafasi kubwa kwenye gazeti hilo.
Mimi kama mpiga kura wa Jimbo la Bukoba Vijijini nataka nimpongeze mbunge wangu huyo kwa kujitokeza na kuonyesha kwamba kumbe bado yupo na bado anayo nia ya kuendelea kuwa mbunge.
Hiyo ni kwa sababu kwa kipindi kirefu wananchi wa Bukoba Vijijini tulishasahau kama tunaye mbunge kutokana na kutomuona mbunge wetu kwa kipindi kirefu wala kumsikia angalau akiongea kwenye vikao vya Bunge kama wanavyosikika wabunge wenzake. Mara ya mwisho kumsikia ilikuwa pale alipojiuzulu uwaziri, kitu kilichotupa fadhaa kwa kutufanya wananchi wa Bukoba Vijijini tuonekane na taifa zima kama watu tusioaminika.
Katika mahojiano hayo Karamagi anaonyesha wazi kitu kilichomfanya akapotea machoni pa wapiga kura wake. Kazungumzia zaidi mafanikio yake binafsi bila kugusia mafanikio yoyote waliyoyapata wapiga kura wake kwa kumfanya yeye awe chaguo lao.
Kitu cha kushangaza ni kwamba kaonyesha tangu mwanzo alivyoweza kuwasaidia na kuwainua wakulima wa zao la kahawa wa Uganda kwa kuwezesha kahawa yao kuuzwa Ulaya kupitia Bandari ya Dar es Salaam badala ya Mombasa.
Lakini mtu yule yule baada ya kuwa mbunge, mwakilishi wa wananchi, hakufanya juhudi zozote za kuwainua wala kuwasaidia kwa njia yoyote wakulima wa kahawa wa jimbo lake, badala yake anatamba na mafanikio aliyoyafikia ya kuwainua wakulima wa zao hilo wa nchi jirani! Tuseme ni watu gani wanaopaswa kujivunia mtu huyo, wananchi wa jimbo la Bukoba Vijijini au Waganda?
Katika mahojiano hayo Karamagi kajionyesha asivyokuwa mwanasiasa bali alichotaka ni kuitumia siasa kufanikisha mambo yake binafsi, kwa matamshi yake anasema ÒÉ.huku mawazo kwamba kwa nafasi yangu niliyo nayo sitapendelea kuwa na nafasi ya uongozi wa kudumu, kwa maana ya ile inayotaka kuwa ofisini muda woteÉÓ
Kauli hiyo moja kwa moja inaonyesha kwamba hata ubunge, huu anaodai ataurudia kwa kishindo, anautaka kwa ajili ya hadhi tu itakayomwezesha kufanikisha mambo yake binafsi kwa urahisi wala si kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, wapiga kura wake, kwa muda wote.
Ikumbukwe kwamba hata watu wanaokuwa watumishi wa umma wanapoutamani ubunge, kwa maana ya kuwatumikia wananchi kwa njia nyingine, inabidi wachukue likizo ili wapate muda wa kuwatumikia wapiga kura wao kwa muda wote, lakini kwa Karamagi hilo ni jambo lisilokubalika.
Kuhusu kujiuzulu uwaziri Karamagi anadai kwamba huko ni kuathirika kimazingira (victim of circumstances). Amekufananisha kujiuzulu huko na mtu kupindukiwa na gari na kufa wakati hakuwa abiria wa gari husika. Hakutaka kuonyesha kwamba kuna watu wanaogongwa na magari kutokana na ulevi wao.
Mtu anayegongwa na gari akiwa amelewa ni vigumu kusingizia tu mazingira ya tukio, maana inawezekana ulevi wake ukawa umemfanya kulala barabarani. Baada ya hilo Karamagi akadai kwamba alijiuzulu baada ya Waziri Mkuu kujiuzulu.
Karamagi hakutaka kuonyesha kwamba kujiuzulu kwa Waziri Mkuu kulisababishwa na nafasi yake aliyokuwa anaishikilia serikalini. Vinginevyo kama suala lingekuwa kwamba Waziri Mkuu akijiuzulu na walio chini yake wanapaswa wajiuzulu basi Baraza zima la Mawaziri ingebidi lijiuzulu wakati ule, isingemlazimu kujiuzulu yeye na Msabaha peke yao.
Kwa hiyo anachotaka kukificha hapa, hasa kwa sisi wapiga kura wake, ni kutaka isijulikane kuwa yeye ndiye aliyemponza bosi wake, Waziri Mkuu.
Mambo mengine ambayo yameonekana kama kuudanganya umma ni yale ya kudai kwamba amefanikisha mpango wa umeme jimboni kwake bila ya kuyataja maeneo yaliyokwishapata huduma hiyo kutokana na juhudi zake.
Alishindwa kufanya hivyo wakati alipokuwa amepewa nafasi ya pekee kwa kufanywa waziri wa nishati, sasa atawezaje kufanya hivyo akiwa mbunge wa kawaida, tena asiyetaka kuifanya kazi hiyo kwa muda wa kudumu?
Madai mengine ni ya kwamba kakamilisha hospitali ya wilaya, tunajiuliza hiyo hospitali imejengwa wapi? Maana hospitali tunazozitegemea, katika jimbo la Bukoba Vijijini, ni zile zinazoendeshwa na taasisi za kidini, hiyo ya Karamagi imejengwa wapi? Tungetaka tuione ili tumpongeze kuliko kuisoma tu kwenye magazeti.
Baada ya kuiangalia nia ya mbunge wetu ya kutaka kuendelea kuwa mwakilishi wetu licha ya kuwepo kwa maswali mengi yanayoizunguka nia yake hiyo, nataka niugeukie utaratibu na kanuni za Chama Cha Mapinduzi uliowekwa kikatiba wa kuwapata wagombea wenye sifa katika chama chetu.
Utaratibu unaoendelea kwa sasa katika jimbo letu la Bukoba Vijijini unatia shaka. Utaratibu huu umeanzishwa na baadhi ya wagombea ukiwa umezipiga kumbo kanuni na taratibu za chama za kuwapata wagombea wanaofaa. Hawa ni watu tunaowatarajia kuwa wangesimama imara kuhakikisha sheria zilizo ndani ya Katiba ya nchi na kanuni za chama zinatekelezwa, sasa cha kusikitisha ndio wamekuwa wa kwanza kuzivunja sheria hizo, tena baadhi yao wakiwa viongozi wakuu walio katika Halmashauri Kuu ya CCM.
Mmoja wa wagombea huu ni mwaka wa tatu tangu tumchague kuwa Mwenyekiti wetu wa Jumuiya mojawapo ya chama ngazi ya wilaya, lakini kazi ambayo amekuwa akiifanya ni ya kutembea kata hadi kata akitoa misaada mbalimbali kwenye shule, zahanati, mipira kwa vijana na misaada kwa vikundi vya akina mama.
Pia amekuwa akinunua kadi za chama na kuzigawa kwenye kata na matawi mbalimbali na hata baadhi ya viongozi wa kata kuzawadiwa vitu mbalimbali kama baiskeli, pikipiki, mashine za kusagia nakadhalika, yakiwa ni malengo yake ili ifikapo kipindi cha uchaguzi aweze kupita kwa urahisi, kuanzia kwenye kura za maoni ndani ya chama.
Hiyo ni pamoja na kuwapeleka baadhi ya viongozi, ngazi ya kata na matawi, kuwatembeza kwenye mbuga za wanyama za Mikumi, Septemba 2008. Ushahidi upo kwenye kalenda za Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Bukoba Vijijini ya mwaka 2009.
Mtu wa pili kwa kukiuka kanuni za chama ni Naziri Karamagi, Mbunge wa sasa. Katika mtazamo wangu pamoja na wanachama wenzangu wa CCM, wenye akili na mtizamo wa kukijenga chama, huyo mtu anatuachia maswali mengi ya kujiuliza.
Sifa yake ya kuwa kiongozi wa chama inatia shaka ingawa tunamshukuru Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyeonyesha uzalendo kwa jimbo letu la Bukoba Vijijini kwa kumchagua kuwa waziri, ingawa baadaye alimuangusha rais kwa kufanya mambo ndivyo sivyo.
Ni vipi Imamu akataze nyama ya nguruwe na iwe halali kwake akiwa muumini wa kawaida wakati imani bado ni ileile? Tulipomchagua Karamagi kipindi kilichopita alipewa uwaziri ukamshinda sasa anataka kuchaguliwa tena akaonyeshe taswira gani aliyokuwa ameisahau?
Tunajiuliza hicho kishindo anachotarajia kurudi nacho bungeni Karamagi anatarajia kukipata wapi? Ndiyo maana tunaishauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuwa karibu na hawa wagombea kwa vile namna wanavyojiamini kunatia shaka.
Haiwezekani mtu ambaye wapiga kura wake wanajiuliza maswali kibao yasiyo na majibu awe na uhakika wa kurudi jimboni kwa kishindo. Hicho kishindo anatarajia kukipataje kama hakuna namna ambayo Takukuru inabidi waifanyie kazi?
Nimalizie kwa kusema kwamba taratibu, kanuni na miiko ya CCM vimekiukwa na kuvurugwa sana hususan na hawa wagomea wawili katika Jimbo la Bukoba Vijijini. Mambo yote yanayoainishwa na chama kwamba ni haramu kufanyika pale mwana CCM anapokuwa anautafuta uongozi ndiyo yamekuwa yakitumiwa na hao watu wawili kama kigezo cha kuwatofautisha na wagombeaji wengine ndani ya chama.
Maana yake ni kwamba mambo yaliyoharamishwa na chama wao wameyahalalisha na kuyafanya nyenzo ya kuwaweka juu ya wenzao. Haramu ya chama ni halali kwao inayowafanya kuwa vinara wa chama!
Uwezo wao mkubwa kiuchumi, ambao bahati mbaya umepigiwa sana kelele na wananchi wote kwa ujumla wakiuhusisha na ufisadi, ndiyo imekuwa silaha yao kuu inayotumika kuwamaliza wanachama wengine ambao wangependa kukitumikia chama na kukiwakilisha kwa uadilifu.
Neno ufisadi linatusumbua sana wana CCM wa jimbo hili la Bukoba Vijijini. Neno hilo linakipaka matope chama chetu. Haiwezekani fisadi awe mmoja ndani ya jimbo lakini jimbo lote lichukuliwe kuwa ni jimbo la mafisadi, au kwamba CCM Bukoba Vijijini ni mafisadi watupu.
Kwanini chama kisijitenge na watu wote wanaohusishwa na kashfa hiyo? Kibaya zaidi ni pale wale wanaohusishwa na kashfa hiyo wanaposhindwa kujificha na badala yake wakaamua kutumia uwezo wao, unaosemekana unatokana na sifa hiyo chafu, kutaka kuwa wawakilishi wa chama na baadaye wawakilishi wa wananchi kwa ujumla! Na tutawezaje kuukana ufisadi iwapo watu hao ndio tutakaoona wanafaa katika kinyangÕanyoro kinachokuja cha Uchaguzi Mkuu? Hivyo ndivyo hali ilivyo katika Jimbo la Bukoba Vijijini, ufisadi unaelekea kushika hatamu.
Hima wana CCM wenzangu, tukiokoe chama chetu kwa kukiepusha na janga hili linalotaka kukikumba. Tuwaangalie wanachama walio waadilifu ndio tuwape uongozi na uwakilishi wa chama.
Wale tunaowaona kwamba uadilifu umewapita pembeni, kama ni marafiki zetu tunaweza kukaa nao tukanywa lubisi na kutafuna kahawa lakini tukikiacha chama chetu salama mikononi mwa watu waadilifu.
Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kuwa ni Kada wa CCM, Irango-Kata ya Butelankuzi, Bukoba Vijijini. Anapatikana kwa simu: O784 304 230.
More Latest News
-
Daladala latumbukia mtoni Dar ABIRIA 21 waliokuwa wakisafiri kutoka Buguruni kwenda Mbagala jijini...
-
Umeyasikia ya Tatu Ntimizi? BAADHI ya wananchi wa Jimbo la Igalula ambao ni wanachama wa Chama...
-
Hispania yaweka historia HISPANIA imekuwa taifa la nane kushinda Kombe la Dunia baada...
- 1
- 2
- 3
- 4
Advertisement

cartoons


