Tuesday, September 07, 2010
   
Text Size

Site Search

rai

Majigambo ya Karamagi yanatoka wapi?

Na Ibrahimu Rwamulaza

GAZETI la Rai toleo namba 871 la Juni 3-9, 2010, lilikuwa limepambwa na habari ya majigambo ya Mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi, iliyokuwa na kichwa cha habari cha ÒNitarudi Bungeni kwa kishindoÓ. Majigambo hayo yametokana na mahojiano aliyofanyiwa mbunge huyo na mwandishi Livingstone Ruhere na kupewa nafasi kubwa kwenye gazeti hilo.

Mimi kama mpiga kura wa Jimbo la Bukoba Vijijini nataka nimpongeze mbunge wangu huyo kwa kujitokeza na kuonyesha kwamba kumbe bado yupo na bado anayo nia ya kuendelea kuwa mbunge.

Hiyo ni kwa sababu kwa kipindi kirefu wananchi wa Bukoba Vijijini tulishasahau kama tunaye mbunge kutokana na kutomuona mbunge wetu kwa kipindi kirefu wala kumsikia angalau akiongea kwenye vikao vya Bunge kama wanavyosikika wabunge wenzake. Mara ya mwisho kumsikia ilikuwa pale alipojiuzulu uwaziri, kitu kilichotupa fadhaa kwa kutufanya wananchi wa Bukoba Vijijini tuonekane na taifa zima kama watu tusioaminika.

Katika mahojiano hayo Karamagi anaonyesha wazi kitu kilichomfanya akapotea machoni pa wapiga kura wake. Kazungumzia zaidi mafanikio yake binafsi bila kugusia mafanikio yoyote waliyoyapata wapiga kura wake kwa kumfanya yeye awe chaguo lao.

Kitu cha kushangaza ni kwamba kaonyesha tangu mwanzo alivyoweza kuwasaidia na kuwainua wakulima wa zao la kahawa wa Uganda kwa kuwezesha kahawa yao kuuzwa  Ulaya kupitia Bandari ya Dar es Salaam badala ya Mombasa.

Lakini mtu yule yule baada ya kuwa mbunge, mwakilishi wa wananchi, hakufanya juhudi zozote za kuwainua wala kuwasaidia kwa njia yoyote wakulima wa kahawa wa jimbo lake, badala yake anatamba na mafanikio aliyoyafikia ya kuwainua wakulima wa zao hilo wa nchi jirani! Tuseme ni watu gani wanaopaswa kujivunia mtu huyo, wananchi wa jimbo la Bukoba Vijijini au Waganda?

Katika mahojiano hayo Karamagi kajionyesha asivyokuwa mwanasiasa bali alichotaka ni kuitumia siasa kufanikisha mambo yake binafsi, kwa matamshi yake anasema ÒÉ.huku mawazo kwamba kwa nafasi yangu niliyo nayo sitapendelea kuwa na nafasi ya uongozi wa kudumu, kwa maana ya ile inayotaka kuwa ofisini muda woteÉÓ

Kauli hiyo moja kwa moja inaonyesha kwamba hata ubunge, huu anaodai ataurudia kwa kishindo, anautaka kwa ajili ya hadhi tu itakayomwezesha kufanikisha mambo yake binafsi kwa urahisi wala si kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, wapiga kura wake, kwa muda wote.

Ikumbukwe kwamba hata watu wanaokuwa watumishi wa umma wanapoutamani ubunge, kwa maana ya kuwatumikia wananchi kwa njia nyingine, inabidi wachukue likizo ili wapate muda wa kuwatumikia wapiga kura wao kwa muda wote, lakini kwa Karamagi hilo ni jambo lisilokubalika.

Kuhusu kujiuzulu uwaziri Karamagi anadai kwamba huko ni kuathirika kimazingira (victim of circumstances). Amekufananisha kujiuzulu huko na mtu kupindukiwa na gari na kufa wakati hakuwa abiria wa gari husika. Hakutaka kuonyesha kwamba kuna watu wanaogongwa na magari kutokana na ulevi wao.

Mtu anayegongwa na gari akiwa amelewa ni vigumu kusingizia tu mazingira ya tukio, maana inawezekana ulevi wake ukawa umemfanya kulala barabarani. Baada ya hilo Karamagi akadai kwamba alijiuzulu baada ya Waziri Mkuu kujiuzulu. 

Karamagi hakutaka kuonyesha kwamba kujiuzulu kwa Waziri Mkuu kulisababishwa na nafasi yake aliyokuwa anaishikilia serikalini. Vinginevyo kama suala lingekuwa kwamba Waziri Mkuu akijiuzulu na walio chini yake wanapaswa wajiuzulu basi Baraza zima la Mawaziri ingebidi lijiuzulu wakati ule, isingemlazimu kujiuzulu yeye na Msabaha peke yao.

Kwa hiyo anachotaka kukificha hapa, hasa kwa sisi wapiga kura wake, ni kutaka isijulikane kuwa yeye ndiye aliyemponza bosi wake, Waziri Mkuu.

Mambo mengine ambayo yameonekana kama kuudanganya umma ni yale ya kudai kwamba amefanikisha mpango wa umeme jimboni kwake bila ya kuyataja maeneo yaliyokwishapata huduma hiyo kutokana na juhudi zake.

Alishindwa kufanya hivyo wakati alipokuwa amepewa nafasi ya pekee kwa kufanywa waziri wa nishati, sasa atawezaje kufanya hivyo akiwa mbunge wa kawaida, tena asiyetaka kuifanya kazi hiyo kwa muda wa kudumu?

Madai mengine ni ya kwamba kakamilisha hospitali ya wilaya, tunajiuliza hiyo hospitali imejengwa wapi? Maana hospitali tunazozitegemea, katika jimbo la Bukoba Vijijini,  ni zile zinazoendeshwa na taasisi za kidini, hiyo ya Karamagi imejengwa wapi? Tungetaka tuione ili tumpongeze kuliko kuisoma tu kwenye magazeti. 

Baada ya kuiangalia nia ya mbunge wetu ya kutaka kuendelea kuwa mwakilishi wetu licha ya kuwepo kwa maswali mengi yanayoizunguka nia yake hiyo, nataka niugeukie utaratibu na kanuni za Chama Cha Mapinduzi uliowekwa kikatiba  wa kuwapata  wagombea wenye sifa katika chama chetu.

Utaratibu unaoendelea kwa sasa katika jimbo letu la Bukoba Vijijini unatia shaka. Utaratibu huu umeanzishwa na baadhi ya wagombea ukiwa umezipiga kumbo kanuni na taratibu za chama za kuwapata wagombea wanaofaa. Hawa ni watu tunaowatarajia kuwa wangesimama imara kuhakikisha sheria zilizo ndani ya  Katiba ya nchi na kanuni za chama zinatekelezwa, sasa cha kusikitisha ndio wamekuwa wa kwanza kuzivunja sheria hizo, tena baadhi yao wakiwa viongozi wakuu walio katika Halmashauri Kuu ya CCM.

Mmoja wa wagombea huu ni mwaka wa tatu tangu tumchague kuwa Mwenyekiti wetu wa Jumuiya mojawapo ya chama ngazi ya wilaya, lakini kazi ambayo amekuwa akiifanya ni ya kutembea kata hadi kata akitoa misaada mbalimbali kwenye shule, zahanati, mipira kwa vijana na misaada kwa vikundi vya akina mama.

Pia amekuwa akinunua kadi za chama na  kuzigawa kwenye kata na matawi mbalimbali na hata baadhi ya viongozi wa kata kuzawadiwa vitu mbalimbali kama baiskeli, pikipiki, mashine za kusagia nakadhalika,  yakiwa ni malengo yake ili ifikapo kipindi cha uchaguzi aweze kupita kwa urahisi, kuanzia kwenye kura za maoni ndani ya chama.

Hiyo ni pamoja na kuwapeleka baadhi ya viongozi, ngazi ya kata na matawi, kuwatembeza kwenye mbuga za wanyama za  Mikumi, Septemba 2008. Ushahidi upo kwenye kalenda za Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Bukoba Vijijini ya mwaka 2009.

Mtu wa pili kwa kukiuka kanuni za chama ni Naziri Karamagi, Mbunge wa sasa. Katika mtazamo wangu pamoja na wanachama wenzangu wa  CCM, wenye akili na mtizamo wa kukijenga chama, huyo mtu anatuachia maswali mengi ya kujiuliza.

Sifa yake ya kuwa kiongozi wa chama inatia shaka ingawa tunamshukuru Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyeonyesha uzalendo kwa jimbo letu la Bukoba Vijijini kwa kumchagua kuwa waziri, ingawa baadaye alimuangusha rais kwa kufanya mambo ndivyo sivyo.

Ni vipi Imamu akataze nyama ya nguruwe na iwe halali kwake akiwa muumini wa kawaida wakati imani bado ni ileile?  Tulipomchagua Karamagi kipindi kilichopita alipewa uwaziri ukamshinda sasa anataka kuchaguliwa tena akaonyeshe taswira gani aliyokuwa ameisahau?

Tunajiuliza hicho kishindo anachotarajia kurudi nacho bungeni Karamagi anatarajia kukipata wapi? Ndiyo maana tunaishauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuwa karibu na hawa wagombea kwa vile namna wanavyojiamini kunatia shaka.

Haiwezekani mtu ambaye wapiga kura wake wanajiuliza maswali kibao yasiyo na majibu awe na uhakika wa kurudi jimboni kwa kishindo. Hicho kishindo anatarajia kukipataje kama hakuna namna ambayo Takukuru inabidi waifanyie kazi?

Nimalizie kwa kusema kwamba taratibu, kanuni na miiko ya CCM vimekiukwa na kuvurugwa sana hususan na hawa wagomea wawili katika Jimbo la Bukoba Vijijini. Mambo yote yanayoainishwa na chama kwamba ni haramu kufanyika pale mwana CCM anapokuwa anautafuta uongozi ndiyo yamekuwa yakitumiwa na hao watu wawili kama kigezo cha kuwatofautisha na wagombeaji wengine ndani ya chama.

Maana yake ni kwamba mambo yaliyoharamishwa na chama wao wameyahalalisha na kuyafanya nyenzo ya kuwaweka juu ya wenzao. Haramu ya chama ni halali kwao inayowafanya kuwa vinara wa chama!

Uwezo wao mkubwa kiuchumi, ambao bahati mbaya umepigiwa sana kelele na wananchi wote kwa ujumla wakiuhusisha na ufisadi, ndiyo imekuwa silaha yao kuu inayotumika kuwamaliza wanachama wengine ambao wangependa kukitumikia chama na kukiwakilisha kwa uadilifu.

Neno ufisadi linatusumbua sana wana CCM wa jimbo hili la Bukoba Vijijini. Neno hilo linakipaka matope chama chetu. Haiwezekani fisadi awe mmoja ndani ya jimbo lakini jimbo lote lichukuliwe kuwa ni jimbo la mafisadi, au kwamba CCM Bukoba Vijijini ni mafisadi watupu.

Kwanini chama kisijitenge na watu wote wanaohusishwa na kashfa hiyo? Kibaya zaidi ni pale wale wanaohusishwa na kashfa hiyo wanaposhindwa kujificha na badala yake wakaamua kutumia uwezo wao, unaosemekana unatokana na sifa hiyo chafu, kutaka kuwa wawakilishi wa chama na baadaye wawakilishi wa wananchi kwa ujumla! Na tutawezaje kuukana ufisadi iwapo watu hao ndio tutakaoona wanafaa katika kinyangÕanyoro kinachokuja cha Uchaguzi Mkuu? Hivyo ndivyo hali ilivyo katika Jimbo la Bukoba Vijijini, ufisadi unaelekea kushika hatamu.

Hima wana CCM wenzangu, tukiokoe chama chetu kwa kukiepusha na janga hili linalotaka kukikumba. Tuwaangalie wanachama walio waadilifu ndio tuwape uongozi na uwakilishi wa chama.

Wale tunaowaona kwamba uadilifu umewapita pembeni, kama ni marafiki zetu tunaweza kukaa nao tukanywa lubisi na kutafuna kahawa lakini tukikiacha chama chetu salama mikononi mwa watu waadilifu.

Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kuwa ni Kada wa CCM, Irango-Kata ya Butelankuzi, Bukoba Vijijini. Anapatikana kwa simu: O784 304 230.

 

Ni mwaka wa uchaguzi wa vijana

Na Muhingo Rweyemamu

KWA vyovyote itakavyokuwa, Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utatawaliwa na vijana, Rai inaweza kuthibitisha.

Tofauti na miaka ya nyuma ambayo siasa za uchaguzi ziliongozwa  na kutawaliwa na wazee huku vijana wakiwa wasaidizi wa ushindi wa wazee hao, mambo yanaonekana kubadilika sana katika uchaguzi wa mwaka huu na vijana wanaonekana kujizatiti na mbinu mpya kuliko watu wa makamo.

Gia aliyoingia nayo Januari Makamba, ya kutembelea Jimbo zima la Bumbuli na kufanya kile wataalam wanaita ‘participatory research’ huku akibuka na kitabu kinachoeleza hali halisi ya wakazi wa Jimbo hilo, ni moja ya mambo yaliyowashitua siyo wagombeaji wenzake tu, bali pia hata vijana waliomo bungeni.

Wakielezea hali hiyo, Ismael Jussa, Mbunge wa kuteuliwa pamoja na Zitto Kabwe, walisema jambo alilolifanya Makamba, limewapa changamoto kama vijana ili waweze kufanya mambo makubwa zaidi ya hayo siku z ijazo.

Takwimu za idadi ya watu, zinatuonyesha kwamba Tanzania ni taifa changa. Kwa maana  kwamba ina idadi kubwa ya watoto na vijana kuliko watu wazima. Kwa mujibu wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, wastani wa umri wa Watanzania ni miaka 18.7 Hii maana yake ni kwamba ukichukua umri wa wazee , ukajumlisha na umri wa watoto , kisha ukagawa mara mbili, umri wa wastani ni miaka 18

Katika Tanzania watoto wenye umri wa chini ya miaka kumi na tano ni milioni 17 wakiwamo wavulana 8,853,529 na wasichana 8,805,810. Wastani wao ni asilimia 43.


Watu wenye umri kati ya miaka 15-64 ni milioni 22 wakiwamo wanaume 10,956,133 na wanawake 11,255,868 na wastani wao ni asilimia 54 ya Watanzania wote wakati wenye umri juu ya miaka 65 wanafanya asilimia 2.9 ya Watanzania kuwa  au kama watu milioni moja na nusu.

Hata hivyo, ukichukua watu wenye umri tangu miaka 0 hadi miaka 29 wanatengeneza asilimia 70 ya Watanzania ambao wengi wao ndiyo kundi kubwa la wapiga kura na hasa wanaopiga kura kwa mara ya kwanza ambao wanaingia katika uchaguzi na vionjo vyao, maono yao na matamanio yao.

Idadi kubwa ya vijana wapiga kura wamo katika Shule za Sekondari za kidato cha tano na sita (1.5) na kutoka Vyuo Vikuu wamo 82,428 ambao wanatarajiwa kuleta hamasa kubwa katika kampeni hizi.

Kihistoria, vijana wamekuwa nguzo muhimu  katika ukombozi wa nchi yetu kupitia TANU, na pia katika kuhakikisha ushindi wa chama hicho na Chama Cha Mapinduzi ambacho ndiyo mrithi wa TANU.

Kwa bahati mbaya, katika miongo ya karibuni, vijana wengi wamekuwa daraja la wazee katika kufikia uongozi. Umoja wa Vijana wa CCM umekuwa ukitumika kuhamasisha watu kupiga kura, kujibu mashambulizi na kwa ujumla kutia hamasa chaguzi za chama.

Miaka ya karibuni, chama hicho kikongwe kilianzisha kikundi cha ‘Tanzania One Theatre Group’ ambacho kwa kiasi kikubwa, kimefanikiwa kuwakusanya Watanzania katika sehemu za kampeni na hivyo kusikiliza hotuba.

Vyama vingine vinejitahidi kuanzisha vikundi ingawa hakuna chama chenye kundi lenye nguvu kama TOT. Hata ndani ya CCM, vikundi vingi vya vijana vimejaribu mara kadhaa kuibuka lakini havikufika mbali.

Safari hii, mambo yamebadilika kabisa, badala ya vijana kuwa wasindikizaji wa wazee, sasa vijana wameamua wenyewe kushika bendera ya chama hicho. Katika sehemu kadha wa kadha, mwitikio  wa vijana umewakosesha raha wazee hata kabla ya kipindi cha kampeni kuanza.

Idadi ya vijana waliochukua fomu kugombea Ubunge na Udiwani kwa tiketi ya CCM ni kubwa mno na kutakuwa na shughuli pevu wakati wa uteuzi.

Sambamba na hilo, ujio wa waziwazi wa wanafunzi wa Vyuo Vikuu katika harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, unaonyesha mabadiliko makubwa yatakayotokea wakati wa kampeni.

Katika mkutano mkuu wa CCM, vijana waliwafunika wazee kwa kila hali. Ukumbi ulikuwa ni wa shamrashamra zilizoongozwa na vijana.

Nyimbo pamoja na hotuba za vijana zilikuwa za mikiki mikiki. Wakati fulani ilionekana kwamba vijana wanataka kuimaliza enzi ya kikundi cha TOT ingawa waswahili walisema uzee ni dawa.

Pale vijana kwa mfano wa Vyuo Vikuu waliposimama kuimba wimbo wao, ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe na kujumuika katika kucheza wimbo huo unaokwenda kwa jina la NI KIKWETE.

Vijana kama Bushoke, Marlow, Flora Mbasha na Doki waliwafanya wajumbe wa mkutano mkuu kushindwa kuketi kwenye viti vyao. Katika kipindi cha burudani hizo, muda pekee wajumbe walipopata nafasi ya kupumzika, ni pale nyimbo za TOT zilipokuwa zikipigwa.

Ujio wa vijana katika kampeni hizi, unatufundisha jambo moja kwamba hali ya sasa ya siasa, ni sawa na jini aliyefunguliwa kwenye chupa. Uwezekano wa kumrudisha ni mgumu na kwa msingi huo, ni lazima tujifunze namna ya kuishi naye.

Mazingira ya zamani ya siasa za nchi zetu, yalikuwa yanatoa nafasi pana kwa viongozi waliomo madarakani kuwa walezi wa vijana wanaochipukia katika uongozi. Kwa sasa, hali hiyo haipo sana. Hivi karibuni, Chama Cha Mapinduzi kilikuwa na semina kule Iringa ambayo ilikuwa ikiwaandaa vijana wake. Hata hivyo, hayo siyo maandalizi ya kisiasa, yalikuwa maandalizi kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu.

Vyama vya upinzani navyo vinao vijana machachari waliokuwamo bungeni na wale waliomaliza shule. Kwa bahati mbaya, habari zao hazisikiki sana kama zinavyosikika zile za CCM na labda sababu kubwa ni ukosefu wa chombo cha kitaifa cha kuwaunganisha na kuwapatia mafunzo vijana. Baada ya siasa kupigwa marufuku katika shule na katika vyuo, vijana wanasiasa wanaokotwa barabarani au wale ambao waliasi amri ya kuzuia siasa katika taasisi za elimu. Kinachoshangaza ni kwamba hata wale vijana wanaochukua kozi za Political Science, hawana muda rasmi ulioruhusiwa kisheria na kitaratibu wa kufanya mazoezi kwa yale wanaotarajia kufanyia kazi.

Kwa nini vijana wanahitaji kuandaliwa? Kwanza kilichojitokeza kule Dodoma ni sababu tosha ya kuwafikirisha wazee na kuwaandaa vijana ili watambue nini cha kuongea, wakiongee lini na wapi.

Kwa mfano katika mkutano huo wa Dodoma, vijana wa Vyuo Vikuu walikaribishwa kusoma risala yao ambayo baadaye tulikuja kupata taarifa kwamba haikuwa imesomwa na yeyote. Yaani ilikuwa risala ya mashtukizi.

CCM ilikuwa imewaalika viongozi wa vyama vya upinzani. Walikuwapo Mwenyekiti Mrema, Mwenyekiti Lipumba na Mwenyekiti Dovutwa pamoja na wengine. Vijana katika hotuba yao, waliwageukia wageni hao ambao kimsingi walikuwa ni wageni wa mwenyekiti wa chama chao, wakasema: “Hawa Mavuvuzela, hawatuwezi”.

Kwa ujumla, maneno hayo yaliwaudhi viongozi wengi wa vyama hivyo. Mmojawao, Profesa Ibrahim Lipumba aliamua kuondoka kabla ya muda wake. Ilipofika muda wa Mwenyekiti kuongea, tofauti kati ya watu waliopata malezi ya kisiasa na wale ambao hawajapata malezi ya kisiasa ilijionyesha. Kikwete aliwakaribisha wageni wake, kuwasifia, kuwapa nafasi ya kuongea na kuwaomba uchaguzi wa mwaka huu uwe wa kistaarabu kwa sababu “tunajenga nyumba moja, hatuna sababu ya kugombania fito”. Hayo ni maneno yaliyosemwa na mtu aliyewakaribisha wageni nyumbani mwake. Mwenyeji, hatarajii watoto wake ‘wawachape fimbo’ wageni wake.

Mwanzo wa ngoma ni lele. Tunatarajia kuyaona mengi wakati wa uchaguzi.

 

Samuel Sitta anatisha

*Ahamishia Ofisi ya Spika wa Bunge Urambo Mashariki
*Thamani yake yamduwaza Kikwete, asema nchi itafilisika

Na Waandishi Wetu

MBUNGE wa Urambo Mashariki, mkoani Tabora, Samuel Sitta, amedhihirisha kwamba yeye ni mtu wa viwango vya hali ya juu, baada ya kuomba Serikali imjengee Ofisi ya Jimbo, yenye hadhi sawa na Ofisi ya Spika iliyoko katika jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyoko Dodoma.

Ofisi hiyo, ambayo ilizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete wiki iliyopita, inaelezwa kuigharimu Serikali zaidi ya Sh milioni 500, kama zitajumlishwa gharama za ujenzi pamoja na samani (furniture) zilizomo ndani ya ofisi hiyo, maalumu kwa ajili ya mbunge wa jimbo la Urambo Mashariki.

Haikuweza kufahamika ni kwanini Sitta, ambaye pia ni Spika wa Bunge linalomaliza muda wake, aliamua kujenga ofisi mpya wakati tayari anayo Ofisi ya Mbunge katika jengo la mkuu wa wilaya ya Urambo.

Rai limeelezwa kwamba kila mbunge, katika mwaka wa fedha wa 2009/2010, alitengewa  Sh milioni 65 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya mbunge jimboni kwake, lakini mbunge wa Urambo Mashariki yeye aliamua ajenge ofisi yenye hadhi ya nafasi yake ya Uspika.

Habari zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya watu walioshuhudia hafla ya uzinduzi wa ofisi hiyo uliofanywa na Rais Kikwete wiki iliyopita, zinasema hata Rais alishitushwa na hadhi ya ofisi hiyo, kiasi cha kujikuta akitamka kwamba ‘kama kila mbunge atataka ajengewe ofisi ya kiwango hiki, basi wabunge wataifilisi nchi hii.’

Jengo la ofisi hiyo ya jimbo, mbali na kuwa na ofisi ya mbunge, inayo pia ofisi ya msaidizi wa mbunge, katibu muhtasi, watumishi wengine wasaidizi (technical staff), chumba maalumu cha watu mashuhuri (vip lounge) na ukumbi wa mikutano unaoweza kuwakusanya watu 30 wakiwa wamekaa kwenye viti.

Rai limefanikiwa kupata baadhi ya nyaraka za mawasiliano baina ya Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhani Khijjah, zinazoelezea uhamishwaji wa fedha kutoka katika vifungu vya maendeleo (fungu 42) kwenda fungu Na 85 cha RAS Tabora ili zikafanye kazi ya ujenzi wa ofisi hiyo.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, Juni 11 mwaka jana, Dk Kashililah alimwandikia barua Khijjah, akijibu barua ya Katibu Mkuu huyo yenye kumb. Na. C/AB/422/01 ya Mei 13, 2009, ambayo ilielekeza kutenga fedha kwenye Fungu 42: Mfuko wa Bunge, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa ofisi ya mbunge wa Urambo Mashariki.

Katika barua hiyo, Dk Kashililah anamuomba Katibu Mkuu Hazina, kuhamisha Sh milioni 200 kutoka Fungu 42 kwenda Fungu 85: Mkoa wa Tabora “kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya mbunge wa jimbo la Urambo Mashariki.”

Kwa mujibu wa barua hiyo, fedha hizo ziliombwa ‘kwa ajili ya kukamilisha ujenzi’ na si kuanza ujenzi, hali inayotafisiriwa na wachambuzi wa mambo ya ujenzi kwamba wakati kiasi hicho cha fedha kikiombwa, tayari mradi huo ulikwishatumia kiasi kingine zaidi ya hicho, kuanzia ujenzi wenyewe, usanifu na uchoraji wa ramani ya jengo.

Pamoja na barua hiyo, ipo barua nyingine ya Juni 4, mwaka huu, ambayo Katibu wa Bunge, Dk Kashililah alimwandikia Katibu Mkuu Hazina, akiomba kuhamishwa Sh milioni 72 kutoka katika fungu hilo la 42 kwenda fungu 85 kwa ajili pia ya ‘kukamilisha ujenzi wa ofisi ya mbunge wa Urambo Mashariki.

“Mradi huo (ofisi ya mbunge wa Urambo Mashariki) haukuweza kukamilika kutokana na upungufu wa fedha zilizopelekwa kupitia Fungu 85: RAS Tabora. Ili kuweza kukamilisha kazi hiyo, naomba kuhamisha kiasi cha Sh 72,000,000 kutoka Fungu 42: Mfuko wa Bunge kwenda Fungu 85: RAS Tabora. Fedha hizo (Sh milioni 72) zihamishwe kutoka vifungu vya maendeleo ambazo hazikuweza kutolewa kutokana na kuchelewa kutekelezwa kwa miradi iliyokusudiwa,” inasema sehemu ya barua hiyo ya Dk Kashililah.

Dk Kashililah amekiri kuwapo kwa mawasiliano hayo baina yake na Katibu Mkuu wa Hazina pamoja na uhamishaji wa fedha hizo kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Bunge ili zikatumike kujenga ofisi hiyo, akisema mradi huo ni sehemu ya miradi ya maendeleo ya Bunge.

Juhudi za kumpata Katibu Mkuu Hazina jana hazikufanikiwa baada ya mtu mmoja katika ofisi yake, aliyejitambulisha kuwa Katibu Muhtasi wake, kuliambia Rai kwamba Katibu huyo, kwa wakati huo tuliopiga simu, alikuwa Ikulu.

Mbali na mamilioni hayo ya Shilingi yaliyotumika katika ujenzi wa ofisi ya mbunge huyo, samani za ofisi (furniture) zilizonunuliwa kwa ajili ya matumizi ya ofisi, zimeigharimu Serikali Sh 100,931,300.00.

Msambazaji wa samani hizo, ambaye alipatikana kwa utaratibu wa wazi kabisa wa zabuni ni M/S Mariedo Home Decor. Huyo naye anatiliwa shaka na baadhi ya wadadisi wa mambo, akidaiwa kuwa mshirika wa karibu wa mbunge wa Urambo Mashariki.

Shaka hiyo, inatokana na ukweli kwamba katika wazabuni wanne waliokuwa wameorodheshwa na Bodi ya Zabuni ya Bunge, M/S Meriedo ndiye aliyekuwa mtu ghali sana, pengine mara mbili ya wengine.

Kwa mujibu wa fomu ya ulinganisho wa bei za Wazabuni (Comparison of Technical Aspects Against Quoted Price), Wazabuni wanne waliokuwa wameteuliwa, bei zao zikiwa katika mabano, ni pamoja na M/S Living Room (Sh 64,769,960.00), M/S Quality Furniture and General Appliance (Sh 49,967,760.00), M/S Mariedo Home Décor (Sh 100,931,300.00 na M/S Alea Industries Ltd (80,462,624.00).

Miongoni mwa mahitaji muhimu katika ofisi ya mbunge huyo, ambayo yanalazimika kununuliwa na Serikali, ni pamoja na kompyuta ndogo (Laptop) ya inchi 17, mashine ya kudurufu karatasi (printer), Televisheni kubwa na ungo wake (Flat Screen TV with Dish), kioo kikubwa na vidude vya kutundikia koti ofisini (Coat hanger).

Aidha, kwenye korido ya kuingilia ofisini kwake, inahitajika seti moja ya viti vya bustanini, stuli 4 na meza ndogo ya bustanini, wakati ukumbi wa mikutano unahitaji kuwekewa meza ya mikutano na viti 24, huku vikihitajika pia viti vya dharura sita pamoja na dawati dogo moja.

Katika moja ya madokezo kati ya Mkurugenzi wa Utawala wa Wilaya ya Urambo (DAD) na wataalamu wake, katika kujadili aina ya samani na gharama zake zinazohitajika kununuliwa kwa ajili ya ofisi hiyo, imeandikwa:

“Baada ya kushirikiana na Msaidizi wa Spika, na kutokana na ‘taste’ ya Mh Spika, gharama ya ununuzi wa samani ni Sh 69,560,000.00 kutoka kwa M/S Mariedo Home Décor. Gharama hizi hazihusishi items zifuatazo: Air Condition, Laptop, kompyuta, photocopy mashine, Fax Machine, Printer na Generator ya 20kv.”

Ofisi hiyo ya mbunge wa Urambo Mashariki, ilizinduliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete, siku chache baada ya kuhutubia Bunge na kuahirishwa, kabla ya kuvunjwa rasmi Agosti Mosi mwaka huu.

Watanzania walio wengi, walioshuhudia hafla ya ufunguzi huo kwa macho na au kupitia matangazo ya vituo vya televisheni nchini, walionyeshwa kushitushwa na ukubwa na ubora wa ofisi hiyo, kiasi cha baadhi ya watazamaji hao kupiga simu chumba cha habari cha gazeti hili, wakisema: “Kumbe Serikali hii ina fedha nyingi, haiwezekani ofisi ya mbunge ifanane na ukumbi wa Bunge Dodoma.”

Wengine walikwenda mbele zaidi na kuhoji: “Kwa nini mbunge, na hasa majimbo ya Urambo awe na ofisi ya gharama kubwa ya namna ile wakati wakazi wa Urambo ni masikini wa kutupwa ikilinganishwa na wilaya nyingine nchini?”

   

CCM yafufua Azimio la Arusha

*Yajipanga kusimamia njia kuu za uchumi
*Yasisitiza elimu ya kujitegemea kwanza
*Yasema bila sayansi Taifa halifiki popte
*Yaagiza Serikali kufumua mitaala ya elimu
*Yakiri wingi wa wasomi umeanza kuwa tatizo

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeufanyia mapinduzi makubwa Mwelekeo wake wa sasa kwa kuamua uwalenge zaidi wananchi wa kipato cha chini ili waweze kushiriki katika mfumo halisi wa uchumi wa dunia ya sayansi na teknolojia.

Sambamba na hayo, Chama hicho kimeangalia kwa kina mwenendo wa uchumi wa dunia, na siasa za hapa nchini na kubaini kwamba kuna kila sababu ya kupunguza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho.

Na ili kufanikisha mambo hayo, CCM imeamua kwamba kuanzia sasa itarejesha mfumo wa Upangaji wa Mipango na Usimamizi wa Uchumi ili kuipa dola nafasi ya kuwa mhimili wa uchumi katika mazingira ya ujenzi wa msingi wa uchumi wa kisasa wa Ujamaa na Kujitegemea katika mazingira ya uchumi wa soko na utandawazi.

Maamuzi hayo yamo katika madokezo yake kadhaa, ambayo yalipitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM kabla ya kuwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliomalizika mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.

Maamuzi hayo, yanaonekana kwamba Tanzania imeamua kufuata mfumo wa uchumi wa China; nchi ambayo Ujamaa pamoja na Ubepari vinafanya kazi sambamba, huku nguvu ya kiuchumi ya mabepari ikisaidia kupambana na umaskini wa walio wengi.

Tangu mageuzi hayo ya kukumbatia mifumo miwili ndani ya nchi moja yaasisiwe mwaka 1978, China imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya uchumi. Mwaka jana, pato la nchi hiyo lilikuwa Yuan trilioni 30.07 ambazo ni sawa na dola za Marekani trilioni 4.287, ikiwa na ongezeko la uchumi la asilimia 9.3.

Mageuzi hayo, yaliletwa na Den Xiao Ping, ambaye alibadilisha mfumo wa Kikomunisti uliokuwa umeitenga China ya Mao Tse Dong na ulimwengu wa nje.

Baada ya mabadiliko hayo, uchumi wa China umekuwa ukikua kwa kasi ya ajabu, kiasi cha kuwa tishio kwa mataifa makubwa kiuchumi kama vile Marekani na Japan.

Katika kijitabu cha CCM cha Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya 2010 hadi 2020, CCM inataja malengo makuu ya mwelekeo huo ambayo yana mambo kama sita hivi.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kupambana kikamilifu na suala la uchumi duni na tegemezi, kwa  kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea, na unaozingatia matumizi ya kiwango cha juu cha maarifa yatokanayo na sayansi na teknolojia.

Ili kuweza kufanikisha jambo hilo, chama kinaziagiza Serikali zake kujipanga kuwawezesha wananchi kiuchumi, kwa kuwapa elimu ya kisasa itakayowawezesha kufanikisha Mapinduzi katika Kilimo na Ujasiriamali.

Chama hicho kinasema ili mkakati wa kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegema, ni lazima itolewe elimu ya kisasa. Na kwa msingi huo, Chama kinaziagiza Serikali zake mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuchungulia upya katika mitaala yake na kuifumua ili kuweza kukumbatia sayansi na teknolojia tangu ngazi ya awali ya mfumo wa elimu.

“Kwa vile uchumi wa kisasa unahitaji watenda kazi wenye ujuzi na maarifa ya sayansi na teknolojia, ni lazima (watenda kazi hao) waandaliwe kwa kupewa elimu bora na ya kisasa,” inasema sehemu ya kijitabu hicho cha Mwelekeo wa CCM.

Aidha, chama hicho kinasema bila matumizi ya elimu ya sayansi na teknolojia, nchi haiwezi kuondokana na uchumi ulio nyuma na tegemezi.

“Kwa hiyo, lazima yafanyike marekebisho katika mitaala ili mafunzo yanayotolewa yapate mwelekeo wa sayansi na teknolojia. Serikali itatilia mkazo uwekezaji wa raslimali katika utafiti na kuufanya utafiti kuwa agenda ya kitaifa kwa kutenga asilimia moja (1%) ya pato ghafi la Taifa, kwa ajili ya utafiti na maendeleo,” inasema sehemu ya kijitabu hicho na kuongeza kuwa lazima Serikali isimamie taratibu za uhawilishaji wa teknolojia na utoaji hakimiliki kwa watafiti na wagunduzi.”

Kwa ujumla, mwelekeo huu unaonyesha dhamira ya CCM katika uwezeshaji wa wananchi mmoja mmoja na katika vikundi.

CCM inasema: “Mkakati mkuu wa uwezeshaji wa kiuchumi wa wananchi, ni ule unaohakikisha kwamba wananchi wenyewe wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yetu ama mmoja mmoja kwa kupitia vyama vyao huru vya ushirika au kwa kupitia kampuni za wananchi ya ubia.

“Wakati huo huo, Watanzania wenye vipaji wataandaliwa katika fani za uongozi wa uchumi na kuwasaidia watu ambao wako tayari kuthubutu kuchukua hatua za kiuchumi. Kuthubutu kiuchumi, ndiyo chimbuko la msukumo katika uchumi wa kisasa.”

Moja ya mambo ambayo yamekuwa yakimhangaisha Rais Jakaya Kikwete tangu alipokuwa akinadi Ilani ya CCM ya mwaka 2005, ilikuwa ni tatizo la uwezeshaji wa watu wenye uwezo wa kuthubutu. Amerudia kusema mara kadhaa na amerudia tena kwenye mkutano mkuu uliomalizika Dodoma, kwamba benki za biashara si rafiki wa masikini.

Kwa maneno mengine, Mwelekeo huuu wa sasa wa CCM umekuja na majawabu juu ya dukuduku la muda mrefu la Rais Kikwete, la kutafuta uwezeshaji wa watu wenye nia ya kuthubutu kufanya mambo makubwa.

Kwa mujibu wa CCM, kwa mtazamo mpana wa Sera ya Uwezeshaji Kiuchumi, aina ya kwanza
ya uwezeshaji ni ile ya mtu mwenyewe kujiwezesha. Yaani mtu anajiwezesha pale anapotambua vipaji alivyonavyo na anaamua kujituma kwa kuvitumia vipaji hivyo.

“Kwa ujumla, elimu yetu hadi hivi sasa imeegemea kwenye kuelimisha watu ili waajiriwe au watumwe. Lazima sasa elimu tunayoitoa kwa vijana wetu
ijielekeze kwenye kuandaa watu wenye kujituma. Wanaojiajiri ni watu wanaojituma.

“Kuna vijana wengi wanaomaliza masomo ya sekondari, ya vyuo na hata vyuo vikuu, lakini hawapati kuajiriwa kwa sababu uchumi haupanuki kwa haraka kiasi. Hivyo jambo jema la nchi kuwa na watu wengi, vijana wengi waliosoma vizuri, sasa limeanza kuwa tatizo kwa nchi

“Kuwa na vijana wengi waliosoma, ni nguvu kubwa kwa Taifa. Ili Taifa liweze kuitumia nguvu hiyo kwa maslahi ya vijana wenyewe na kwa maendeleo ya kiuchumi na jamii ya nchi yetu, CCM itazitaka Serikali kuibua Mpango Kabambe wa kuwawezesha kiuchumi vijana wasomi walio tayari kujituma kwa kujiajiri ili watumie nguvu na maarifa waliyonayo,” CCM inaagiza.

Je; ni mpango gani umeandaliwa kwa vijana hawa? Chama hicho kinasema kwamba Serikali italazimika kuwapa mafunzo ya ujasiriamali na yanayohusu shughuli wanazokusudia kuzifanya, lakini pia Serikali iweke utaratibu mwepesi wa kupata mikopo nafuu.

Chama hicho kinasema wale wote watakaokuwa na nia ya kushiriki katika mpango huo, washauriwe kuunda chombo chao cha kushauriana.

“Utaratibu wa aina hii, wa kuwawezesha wasomi na wataalamu kujiajiri, una manufaa mawili kwa Taifa. Kwanza, unatoa ajira ya uhakika kwa wahusika na hivyo kuipunguzia nchi tatizo la watu kukosa ajira na madhara yake, na pili; unawezesha wasomi kutoa mchango chanya katika kujenga uchumi wa kisasa na kuongeza utajiri wa nchi,” inasomeka sehemu ya kijitabu hicho.

Chini ya utaratibu wa kuwawezesha wasomi, wajasiriamali, wafanyabiashara wa kati na wa juu, CCM inaziagiza Serikali zake kuandaa mkakati wa kibenki ambao utawezesha upatikanaji wa mikopo kwa makundi yote hayo.

“Benki nyingi tulizonazo sasa kwa aina ya shughuli zao, ni benki za kibiashara zaidi kuliko zile za kuendeleza sekta za uzalishaji mali, hususan kilimo. Aidha, hutoza riba kubwa. Hivyo ni muhimu Serikali ikahakikisha kuwa kwa makusudi, vinaanzishwa vyombo vya fedha ambavyo vitasaidia kuwawezesha wananchi kwa riba nafuu kuliko ilivyo sasa, ikilenga uanzishwaji wa Benki ya Kilimo, Benki ya Kuendeleza Viwanda na Benki ya kutoa mikopo ya muda mrefu ya ujenzi wa nyumba,” inaagizwa.

 

Shein aanza vizuri

*Kisumo, Balozi wa Kenya wataka wapinzani wajifunze CCM

Na Waandishi Wetu

KUTEULIWA kwa Dk Ali Mohamed Shein kuwa mgombea urais wa Zanzibar pamoja na Dk Mohamed Gharib Bilal kuwa mgombea mwenza, kumeelezwa kwamba ni ukomavu wa hali ya juu wa kidemokrasia na kisiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete.

CCM, katika vikao vyake vilivyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita, kilimpitisha Dk Shein kuwa mgombea urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, huku pia chama hicho kikimpitisha Dk Bilal kuwa mgombea mwenza, uteuzi uliowashangaza wengi wa wafuatiliji wa masuala ya kisiasa ndani ya CCM.

Dk Bilal alikuwa miongoni mwa wateule watano waliopendekezwa na Kamati Kuu Maalumu ya Zanzibar kugombea urais wa visiwa hivyo, kabla ya kuibuka tena katika tatu bora ambayo Kamati Kuu ya CCM iliwasilisha majina yao mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa uteuzi wa mwisho. Majina hayo matatu ni ya Dk Shein, Dk Bilal na Shamsi Vuai Nahodha.

Katika upigaji kura uliofanywa na wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, Dk Shein aliibuka mshindi dhidi ya wenzake hao baada ya kujikusanyia kura 117, huku Dk Bilal, ambaye naye alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kushinda akipata kura 53 na nyingine 33 zikienda kwa Nahodha. Watatu wote hao ni wajumbe wa Kamati Kuu.
 
Uteuzi wa Bilal kuwa mgombea mwenza, uliofanywa na Rais Kikwete, unaweza kuwa na maana nyingi, lakini kubwa moja ni kuimarisha mshikamano ndani ya CCM yenyewe-Bara na Visiwani.

Maana nyingine pana, ni kuwa kuteuliwa kwake kumepoza hali ya kisiasa ya Zanzibar ambayo ilianza kuchafuka hata kabla vikao vya uteuzi havijaanza kukaa.

Dalili za Dk Bilal kuteuliwa kuwa mgombea mwenza zilianza kujionyesha saa 10 jioni baada ya wajumbe wa mkutano mkuu kuingia katika ukumbi wa Kizota ili kuanza mkutano wao baada ya mapumziko kwa ajili ya kupata chakula cha mchana.
 
Katika kipindi hicho cha kati ya saa 10 na saa 11, Dk Bilal akiwa ameketi katika kiti chake eneo ambalo lilikaliwa na Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alifuatwa na mmoja wa walinzi wa Rais Kikwete na kutoka naye nje hadi katika jengo lililoko pembezoni na ukumbi huo wa Kizota, jengo ambalo Rais na watendaji wake waandamizi walikuwa wakilitumia kama ofisi na sehemu ya kupatia maakuli.

Kitendo hicho kilitokea wakati Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba akiwa tayari ameingia ukumbini na kutoa tamko ambalo liliwataka wasanii waliokuwa wakiwaburudisha wajumbe waendelee na kutoa burudani hiyo akisema Mwenyekiti wa CCM alikuwa bado na dharura iliyomzuia kuingia ukumbini muda huo. Baada ya dakika kama 10 hivi, Dk Bilal alirejea tena ukumbini, huku akionekana kama mtu aliyezongwa na mawazo.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu, aliliambia Rai kwamba baada ya Rais Kikwete kukutana na wajumbe hao, alitaja jina la Dk Bilal na kuwaomba waridhie chaguo lake hilo kabla ya kuwapatia maelezo ni kwanini anadhani mwanachama mwenzao huyo anafaa kwa nafasi hiyo kwa maslahi ya nchi na ya chama chenyewe.

Kwa mujibu wa mjumbe huyo wa Kamati Kuu, karibu wajumbe wote waliokuwamo katika kikao hicho cha dharura, ambacho kiliitishwa na Mwenyekiti, Kikwete, katikati ya mkutano mkuu wa CCM, waliridhika na sababu na maelezo ya mwenyekiti huyo, na hivyo Dk Bilal kupitishwa bila kupingwa na yeyote. 

Wachambuzi wa hali ya siasa ilivyo kwa sasa nchini, wanasema CCM ilihitaji kwanza kushikamana yenyewe kama ilivyofanya katika mkutano mkuu wake wa Dodoma kabla ya kuingia katika Uchaguzi Mkuu ujao, ndipo sasa iendeleze juhudi zake za kuimarisha muafaka wa kisiasa baina yake na Chama cha CUF.

Wanasema uteuzi wa Dk Shein na Bilal, umetoa picha ya dhahiri katika mwelekeo wa CCM ya leo na kesho, katika kuhakikisha kwamba siasa za chuki, uhasama na visasi baina ya wana-CCM wenyewe na baina ya CCM na CUF, zinafutika ili kuijenga Zanzibar moja yenye amani na mshikamano katika nyanja zote za maisha ya binadamu.

“Neno moja tu ninaloweza kuzungumza katika uteuzi wote huo, ni kwamba Dk Shein ameanza vizuri hata kabla hajaingia Ikulu ya Zanzibar. Amerahisishiwa ushindi kwa sababu CCM wanarudi Zanzibar wakiwa kitu kimoja.

“Hii tu imeonyesha kuwa CCM ni chama cha mfano katika jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, kwa maoni yangu nadhani hicho ndicho chama kinachoweza kutuunganisha wote katika jumuiya hii,” anasema Balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso katika maoni yake kwa Rai juzi Jumanne juu ya uteuzi wa Dk Shein na Dk Bilal na kuongeza:

“Kwa uteuzi wa Dk Shein na Bilal, kwanza, CCM imewaleta pamoja wanachama wake wa Zanzibar. Pili, imezidi kuimarisha zaidi Muungano. Kwa kweli Mwenyekiti wake (wa CCM-Jakaya Kikwete) na viongozi wenzake wameonyesha busara kubwa na ukomavu wa kidemokrasia.

“Na demokrasia hiyo, haiishii kwa uteuzi huo tu, bali hata kitendo cha kuwapa nafasi viongozi wa upinzani kama kina Mrema (Augustine Mrema-Mwenyekiti wa TLP), kuhutubia katika mkutano mkuu, umekifanya CCM kuwa cha mfano katika ukanda huu wa Afrika Mashariki…hii ni changamoto kwa vyama vingine vya upinzani, vinapaswa kuiga na kuimarisha demokrasia kama hii ndani ya vyama vyao.”    

Kwa upande wake, mmoja wa wakongwe wa siasa nchini, Peter Kisumo, akitoa maoni yake kuhusu Mkutano Mkuu wa Dodoma, anasema: “Sisi ni Taifa moja lenye mshikamano wa kweli. Mkutano wa Dodoma umedhihirisha kwamba huu ulikuwa mkutano wa kitaifa, na si wa makundi ya watu. Nasema haya kwa sababu nimekaa kwenye NEC miaka 30, nayajua haya mambo.

“Tunachohitaji kwa sasa ni political investment (dhamira ya kisiasa) kuvunja udini. Umoja wa kitaifa chini ya utawala wa CCM tunao, na tatizo letu si ukabila tena, bali ni udini. Ndiyo maana Rais Kikwete, katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano mkuu, anasema ‘hatutakubali kabisa mtu anayetaka kuligawa Taifa kwa misingi ya kidini.’

Akitoa maoni yake kuhusu Ilani ya Uchaguzi ya 2010-2015, na Mwelekeo wa CCM katika miaka 10 ijayo (2010-2020), mkongwe huyo wa siasa anasema chama chochote cha siasa, kiwe chama tawala au cha upinzani, kukubalika kwake kwa wananchi, lazima kutokane na programu yake ya maendeleo.

Anasema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, CCM itashindana na vyama visivyo na programu yoyote ya maendeleo ya nchi, iwe ya miaka mitano au 10 ijayo, na badala yake vyama hivyo vimejaa porojo tu.

“Position (nafasi) hii ambayo CCM imeionyesha (katika Ilani na Mwelekeo), ni ukomavu wa kifikra. Kwanza, CCM kina malengo yake kama yalivyofafanuliwa wazi (na Kingunge Ngombare-Mwiru) katika mkutano mkuu, malengo ambayo baadaye yatapimwa na watu,” anasema Kisumo na kuongeza:

“Kinachotokea leo kwa wale wanaobabaisha, wanataka kuiba sifa na programu za CCM juu ya elimu, mawasiliano, barabara na kadhalika. Hili unaweza kuliona kwa wabunge wa upinzani, ambao kwao kuna shule na zahanati zimejengwa na Serikali, lakini wanajitapa kwamba ni wao waliozijenga.

“Chadema, wakitaka kujisifu, waje na programu yao inayoizidi ya CCM ili wawe ‘The Government in waiting’ (Serikali kivuli). Waje na kitu tukione. Programu hii iliyokwisha (Mwelekeo wa CCM-2000-2010), ndiyo imejenga shule nyingi na zahanati kwa kila kijiji, bila kujali jimbo fulani liko mikonani mwa CCM au la.

“CCM ina sera za usawa kwa kata zote, wilaya zote na sera za usawa kwa watu wote, lakini hadi leo hatujawahi kuona mipango na sera za vyama vingine ili watu wazipime na kuzinganisha.”

   

Page 1 of 5

More Latest News

  • 1
  • 2
  • 3
  • 4

cartoons



Who's Online

We have 9 guests online

Login Form