Friday, September 10, 2010
   
Text Size

Site Search

bingwa

Humud akwama kwenda Urusi

NA TIMZOO KALUGIRA

MABINGWA wa soka wa Ligi Kuu ya Bara, Simba ya Dar es Salaam wanadaiwa kuzuia kiungo wao, Abdulhalim Humud kwenda nchini Urusi kufanya majaribio ya soka la kulipwa.
Habari ambazo Bingwa imezipata kutoka kwa mtu wa karibu na mchezaji huyo zinadai kwamba kuna timu nchini Urusi ilikuwa ikimtaka mchezaji huyo lakini viongozi wake walimkatalia.
“Jambo hili lilimkera mno Humud ameonekana kukosa raha baada ya kukataliwa kwenda kusakata kandanda huko Urusi, aliwambia viongozi wake kuwa kama vipi waongee na timu hiyo wapande dau kwa kulipa mkataba aliokuwa nao lakini walimkatalia,” alisema mtoa habari hiyo.
Mtoa habari hiyo aliliarifu Bingwa kuwa kutokana na kuwa na mkataba na klabu hiyo ilimbidi akubaliane na hali halisi kwani hakuna kiongozi hata mmoja aliyekuwa tayari kushughulikia suala lake.
Bingwa lilimtafuta Humud ili kuzungumzia suala hilo lakini mchezaji huyo alisema kuwa kwa sasa hayuko tayari kuzungumzia mambo hayo na anachokiangalia ni msimu mpya wa ligi inayotarajia kuanza Agosti mwaka huu.
Hata alipobanwa na Bingwa, mchezaji huyo badala yake alionekana kuihimiza kamati ya usajili ya klabu hiyo, kusajili wachezaji wa maana wanaoweza kuisaidia timu iweze kutetea ubingwa msimu ujao.
“Kamati iangalie ni wapi palikuwa na mapungufu timu ilipokuwa uwanjani katika msimu uliopita, ili kuweza kusajili wachezaji wanaoweza kuziba pengo hilo na kuleta maendeleo katika klabu yetu,” alisema Humud.
Bingwa lilizungumza na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage ambaye hata hivyo alisema kwamba hangependa kuzungumzia vitu visivyo rasmi.
“Hayo mambo si rasmi kwa hiyo sina habari yoyote kuhusu hilo na siwezi kuzungumza chochote,’’ alisema.

 

Kipa mpya Yanga kutua leo

NA TIMZOO KALUGIRA

MRITHI wa kipa namba moja wa Yanga, Obren Curkovic anatarajia kutua leo akiwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mserbia Costadin Papic.
Kipa huyo ambaye pia kutoka Serbia anaitwa Knezevic Ivan anakuja baada ya Obren kumaliza mkataba wake na klabu hiyo na kukataa kuongeza.
Obren aliondoka hapa nchini mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2009/2010.


Habari za kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo zilisema kuwa wakati Papic akiwa likizo alimtafuta kipa huyo ili kuja kuwa na mlinda mlango wa uhakika.
 “Kipa huyo anakuja kesho (leo) na kocha hivyo atafika na kusaini  mkataba ingawa bado sijajua atasaini mkataba wa miaka mingapi,” kilisema chanzo hicho.


Aidha alisema kuwa baada ya kutua kocha, timu inatarajia kuanza mazoezi keshokutwa.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Yanga Lawrance Mwalusako, jana alizindua tawi la Yanga Lango la Jiji ambalo litatumia jina la mpira mbinu.
Hata hivyo wakati wa uzinduzi wa tawi hlo hakukuwa na shamra shamra sana na badaka yake wanatarajia kufanya sherehe hapo baadaye.



 

Blatter amuonya rais Sarkozy

*Aziomba radhi FA za England, Mexico kutokana na makosa ya waamuzi
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
RAIS wa FIFA, Sepp Blatter ameonya kuwa Ufaransa inaweza kufungiwa kushiriki soka la kimataifa iwapo serikali itaingilia uendeshaji wa timu ya taifa.
Blatter alisema ametuma "ujumbe wa wazi” kwa Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, aliyeishutuma timu ya Ufaransa kwa kuonyesha kiwango cha chini kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Sarkozy aliahidi kuongoza uchunguzi wa kilichosababisha timu hiyo kuboronga.
Lakini Blatter alisisitiza mabosi wa soka duniani, Fifa, inapinga: "… uingiliaji wa kisiasa, hata kama ni katika ‘level’ ya urais."
Ufaransa ilimaliza ikiwa ya mwisho kwenye kundi lao huku ikiandamwa na matatizo ya ndani na nje ya uwanja.
Mshambuliaji Nicolas Anelka alitimuliwa kikosini baada ya kugoma kumwomba radhi kocha Raymond Domenech waliyebadilishana maneno makali.
Kikosi kilichosalia kiligomea mazoezi kupinga kutimuliwa kwa Anelka huku nahodha Patrice Evra akitukanana na kocha wa viungo, Robert Duverne.
Sarkozy aliamuru kufanyike marekebesho makubwa ndani ya FA ya nchi hiyo (FFF) na tangu timu irejee, amekwishafanya mazungumzo na nahodha wa zamani, Thierry Henry, huku Jean-Louis Valentin akiachia nafasi ya urais ya FFF.
FFF imekwisha omba radhi kwa mashabiki lakini Blatter alisema uingiliaji wa serikali katika masuala ya soka, hautavumiliwa.
"Ufaransa wanafanya mazungumzo na serikali lakini soka lazima libaki mikononi mwa shirikisho. Tutawasaidia kutatua hili na ikishindikana, tutaifungia nchi hiyo.
"Niseme wazi, kuingiliwa na siasa kwenye soka kutashughulikiwa na Fifa bila kujali serikali imeingilia namna gani au hata ukubwa wa nchi husika,” alisema Blatter. 
Wakati huo huo, Blatter ameiomba msamaha FA ya England kutokana na kukataliwa kwa bao la Frank Lampard.
Bao hilo la wazi lilikuwa la kusawazisha katika pambano la Kombe la Dunia hatua ya 16 bora dhidi ya Ujerumani wakati Ujerumani ikiongoza kwa mabao 2-1.
Shuti la mbali la Lampard liligonga mtambaa panya na kudunda ndani ya mstari wa goli lakini waamuzi wakalikataa na sekunde chache baadaye, marudio ya TV yalionyesha kuwa lilikuwa halali.
"Na sasa ni wazi kutokana na matatizo tuliyoyashuhudia kwenye Kombe la Dunia, itakuwa ni upuuzi kutoanzisha mjadala wa matumizi ya teknolojia wakati tutakapokutana Julai,” alisema Blatter.
Alikiri kuwa amekwisha zungumza na FA za England na Mexico kuhusu makosa ya waamuzi yaliyozigharimu timu zao na kuwaomba msamaha.

   

Ronaldo: Nani Drogba, hatumuogopi

OHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

CRISTIANO Ronaldo amesema kwamba Ureno haina hofu yoyote dhidi ya Didier Drogba wakati timu zao zitakapomenyana kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.
Winga huyo, alisema kikosi chake kipo imara na kitashuka dimbani kumenyana na Ivory Coast inayoongozwa na Drogba kwa dhamira moja ya kupata ushindi.
Timu hizo zitashuka dimbani leo kumenyana katika Uwanja wa Port Elizabeth, kabla ya wapinzani wao wengine kwenye Kundi G, Brazil kukipiga na Korea Kaskazini.
"Tunafahamu kila kitu kuhusu Drogba, ni mchezaji mahiri," alisema Ronaldo.
"Lakini hatuwezi kumuogopa. Tutaweka nguvu zetu kwenye timu, mbinu na lengo letu. Hiyo ni njia pekee ya kupata ushindi."
Ureno imefuzu michuano hiyo baada ya kucheza mechi ya mtoano dhidi ya Bosnia-Hercegovina.
Lakini, Ronaldo alisisitiza kwamba kipindi hicho kigumu kimeshapita kwa upande wao na timu hiyo iliyofika nusu fainali ya fainali za Kombe la Dunia 2006 imepania kufanya vyema Afrika Kusini.
"Kitu muhimu ni kuvuka raundi ya pili na kama ikiwezekana ni kuwa vinara kwenye kundi, hiyo ni bora zaidi," alisema Ronaldo, 25.
"Kama sivyo, tutacheza na Hispania, na pia hatutakuwa na hofu nao. Hispania ni moja ya timu inayopewa nafasi ya Kombe la Dunia, lakini sisi hatumhofii yeyote. Tunakwenda kucheza na kushinda mechi, au kuibuka mabingwa."

 

Tshabalala atangaza vita Bafana


JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

KIUNGO wa Afrika Kusini, Bafana Bafana, Siphiwe Tshabalala, anasema mechi yao dhidi ya Uruguay ni ya lazima ushindi kama wanahitaji kuendelea kwenye michuano ya Kombe la Dunia.
Bafana ilifungua michuano hiyo Ijumaa iliyopita kwa sare ya 1-1 na Mexico katika mechi zao za Kundi A linaloundwa pia na timu za Ufaransa na Uruguay. 
Tshabalala ndiye alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao katika fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini katika sare hiyo dhidi ya Mexico.
"Mechi dhidi ya Uruguay ni ya lazima ushindi wa kwetu," alisema Tshabalala.
"Tutakwenda kupambana kwa nguvu zote na tunaamini taifa zima litakuwa nyuma yetu. Naamini tutafanya vizuri zaidi katika mechi yetu ya pili.
"Mechi dhidi ya Mexico imeshapita na sasa nguvu zetu zipo kwa Uruguay. Tunafahamu kwamba itakuwa ngumu, lakini tutapigana kwa nguvu zote kwa taifa letu.
"Presha imekuwa kubwa kutokana na mechi hiyo. Tumeonyesha uchu wa kuibuka na ushindi. Tunafahamu Uruguay wanacheza soka gumu na wana wachezaji mahiri kama Diego Forlan."
Kiungo huyo wa Kaizer Chiefs, anaanza kuzitoa udenda timu za Ulaya na kuwa miongoni mwa wachezaji waliofunga mabao bora katika kikosi hicho cha Bafana.
"Lazima nithibitishe kwamba hiki ni kipindi changu bora katika maisha yangu ya soka. Awali nilikuwa siamini kabisa nitakachoweza kufanya, lakini nilipogundua kwamba naweza, nililia. Nafikiri bado naweza kushinda na nina furaha kwa kiwango changu," alisema.
"Ni furaha kubwa kwangu kufunga bao la kwanza la michuano hii. Nilifurahia sana mechi ile kwa kuwa ilikuwa ya 50 kwangu, na natarajia mengi zaidi.
"Siku zote nimekuwa nikipiga mashuti golini kwa dhamira ya kufunga na najiona kama mwenye bahati kwa kufunga bao lile muhimu na la kukumbukwa. Lakini ni suala la timu nzima, inapaswa pongezi kwa jinsi walivyopigana."

   

Page 1 of 6

More Latest News

  • 1
  • 2
  • 3
  • 4

cartoons



Who's Online

We have 9 guests online

Login Form