Dunga amsikitikia Maximo
Na Dominic Isiji
KOCHA mkuu wa timu ya soka ya Brazil, Carlos Dunga, ameeleza kusikitishwa kwake na kuondoka kwa kocha mkuu wa timu ya Tanzania, Taifa Stars, Marcio Maximo ambaye mkataba wake unakamilika mwezi ujao.
Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemtangaza Jan Poulsen raia wa Denmark kama mrithi wa Maximo na ataingia mkataba wa miaka miwili Agosti Mosi mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi baada ya mechi ya kihistoria kati ya Taifa Stars na mabingwa wa dunia mara tano, Dunga alisema Maximo amefanya kazi kubwa kuibadilisha Taifa Stars.
“Ninampongeza Maximo kwa kazi nzuri aliyofanya kwa timu hii (Taifa Stars) ila cha kusikitisha ni kwamba anamaliza muda wake,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Brazil.
Dunga alikiri kufurahishwa na mchezo wa juzi ambao Brazil ilishinda 5-1 akisema kuwa alihitaji kucheza na timu yenye kasi.
Alisema kuwa Maximo ameweza kutengeneza timu nzuri yenye kucheza na mipango na kwa kasi jambo ambalo liliwapa taabu mabeki wake na wakati mwingine kufanya washindwe kupanda wakihofia kuzidiwa kasi kwa mashambulizi ya kushitukiza.
Katika mchezo wa juzi, Brazil ilitumia kikosi chake cha kwanza ambacho kilimkosa mchezaji mmoja tu, kipa Julio Cesar anayeuguza jeraha ya mgongo na alishindwa kusafiri na timu hiyo kuja Dar es Salaam.
Dunga alisema kuwa nia ya Brazil kucheza na Zimbabwe na Tanzania kama maandalizi yao kuelekea Kombe la Dunia linaloanza kesho kutwa nchini Afrika Kusini, ilikuwa ni kujipima nguvu na kasi ya timu pinzani hususan za Afrika.
“Nchi za Afrika zinasifika kuwa na wachezaji wenye nguvu na kasi na nimeridhika na michezo yetu miwili ya kimataifa ya kirafiki kwa sababu Zimbabwe walicheza mpira wa nguvu na Tanzania mpira wa kasi vitu ambavyo wachezaji wangu waliweza kuvimudu,” alisema.
Hadi mechi ya juzi, Brazil mara ya mwisho kwa nyavu zao kutikiswa ilikuwa Oktoba mwaka jana ambapo walishinda 2-1 katika mchezo wao wa kufuzu kuelekea Kombe la Dunia.
Maximo
KOCHA mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, anayemaliza muda wake Marcio Maximo amesema kuwa mrithi wake atapata kazi rahisi.
Nafasi ya Maximo itachukuliwa na Jan Poulsen raia wa Denmark ambaye anatarajiwa kuingia mkataba wa miaka miwili Agosti 1 mwaka huu.
Akizungumza baada ya mechi ya juzi kati ya Taifa Stars na Brazil uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Rais Jakaya Kikwete, Maximo alisema mrithi wake hatakuwa na shida ya kuanza kuunda kikosi.
Alisema kuwa anaondoka huku akimwachia Poulsen kikosi imara cha Taifa Stars na timu nzuri za vijana.
“Sidhani kama (mrithi wangu) atapata shida na ninategemea kuwa atayaendeleza mazuri niliyoanzisha ila kama atataka kuanza upya, hiyo itakuwa jukumu lake,” alisema Maximo huku akimtakia kila la heri Poulsen .
Akizungumzia kuhusu mechi ya juzi, Maximo alisema amefurahishwa na wachezaji wake licha ya kwamba walilazimika kucheza michezo miwili muhimu ndani ya saa 24.
Stars walifunga na Rwanda 1-0 Jumapili jijini Kigali na kuyaaga michuano ya Kombe la Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) kwa jumla ya mabao 2-1 na siku iliyofwata wakafungwa 5-1 na mabingwa wa dunia mara tano Brazil katika mechi ya kihistoria.
Maximo alisema ijapokuwa anaondoka, matarajio yake ni kwamba Taifa Stars itacheza mechi nyingi za kirafiki kama ile ya Brazil ili kuwakomoza wachezaji.
Alisema kuwa mechi dhidi ya Brazil ilikuwa darasa tosha ya ni nini kinachotakiwa kwa wachezaji ili nao pia waweze kucheza soka la kulipwa.
Manji! Ee bwana ee!
*Anunua tiketi za Sh milioni 90 kwa ajili ya wanachama wa Yanga kuiona Stars ikikipiga na Brazil wiki ijayo
Na Mwandishi Wetu
HATIMAYE ahadi ya mdhamini wa klabu ya Yanga, Yusuph Manji imetimia na sasa wanachama 3,000 wa klabu hiyo wana uhakika wa kuiona mechi kati ya Taifa Stars na Brazil Jumatatu ijayo.
Mfanyabiashara huyo kijana jana alinunua tiketi hizo zinazouzwa kwa Sh 30,000 kila moja hivyo kuwa na jumla ya thamani ya Sh milioni 90, zitakazogawiwa kwa wanachama watakaohudhuria Mkutano Mkuu wa utakaojadili rasimu ya Katiba ya klabu hiyo, Jumatatu ijayo kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay.
Barua aliyomwandikia Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), yenye kumbukumbu namba Yanga.TR/ 042.010 ya jana, inaonyesha kuwa Manji anaiomba TFF kumpatia tiketi 3,000 kwa ajili ya wanachama wa Yanga ili wakaishangilie timu ya taifa itakapocheza na Brazil.
Ni wazi kuwa TFF ililikubali ombi hilo kwani Manji alipa fedha kwa ajili ya tiketi hizo kwenye tawi la CRDB, Pugu Road jijini hapa.
Manji alilipa kwa hundi ambazo nakala zake tunazo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mdhamini mmoja kununua idadi kubwa namna hiyo ya tiketi.
Hii si mara ya kwanza kwa ‘kibopa’ huyo kufanya kufuru kwani alipokuwa mfadhili wa Yanga, aliwahi kuwaingiza bure mashabiki wa timu hiyo kwenda kuishangilia timu yao ilipokuwa ikicheza mechi moja ya kimataifa kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza.
Kitendo hicho cha Manji ni katika harakati zake za kuhakikisha mkutano huo muhimu utakaotengeneza njia ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa klabu hiyo, unafanikiwa huku ukiwa wa amani.



